MKATABA, HATI NA MAMBO 11 YA MUUNGANO
Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume, Aprili 22, 1964, Zanzibar.
Ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi Aprili
26, 1964, na Aprili 27, 1964 viongozi hao walikutana katika ukumbi wa
Karimjee, jijini Dar es Dalaam kubadilishana hati za Muungano.
Sheria za Muungano ilitamka kwamba, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri
ya Watu wa Zanzibar zililazimika, kuwa dola ya Jamhuri kwa jina la
Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, jina ambalo
lilibadilishwa Oktoba 28, 1964 na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa kupitia sheria ya Jamhuri ya Muungano, sheria namba 61, ya mwaka
1964.
Msingi wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na
katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ni Hati za Muungano za Mwaka 1964.
Hati za Muungano zilitiwa saini na Nyerere na Karume, Aprili 22,
1964 na hapo Tanganyika na Zanzibar kuwa dola moja kwa misngi
inayotambulika kimataifa. Baada ya kuungana, Mwalimu Nyerere alikuwa
rais wa kwanza na Karume alikuwa makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Aprili 26, 1964, bunge la Tanganyika lilipitisha sheria za
Muungano, ambazo baadayezilithibitishwa na Baraza la Mapinduzi Zanzibar.
Mnamo Aprili 27, 1964 waasisi wa Muungano walibadilishana Hati za
Muungano na wajumbe saba wa Baraza la Mapinduzi waliapishwa kuwa wabunge
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Watanganyika na Zanzibar ambao ni Amani
Karume, Kassim Abdallah Hanga, Abdulrahman Babu, Hassan Nassor Moyo,
Aboud Jumbe, Hasnu Makame na Idris Abdul Wakil. Kati yao, Aboud Jumbe na
Hassan Nassor Moyo wangali hai.
Katiba ya muda ya mwaka 1965 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ilianisha mambo 11 ambayo yalikubalika kuwa ni ya Muungano ambayo ni;
Katiba na Serikali ya Muungano, Mambo ya nchi za nje, Ulinzi, Polisi,
Mamlaka juu ya mambo yanayohusika na hali ya hatari, Uraia, Uhamiaji,
Mikopo na Biashara za nje, Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya
Muungano, Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru
wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa Tanzania unaosimamiwa
na idara ya forodha, Bandari, mambo yanayohusika na usafiri wa anga,
posta na simu.
Katiba ya muda ya mwaka 1965 ilianisha utawala wa serikali ya mfumo
wa chama kimoja, TANU kwa Bara na ASP kwa Zanzibar. Katiba hii,
ilizingatia misingi ya makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 na sheria
za Muungano wa Tangayika za Zanzibar.
Katiba hiyo ilianisha serikali mbili, uwakilishi wa Zanzibar katika
bunge la Muungano ikiwa na mamlaka juu ya mambo yote ya Muungano na
mambo yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanganyika. Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa na mamlaka juu ya mambo yote yasiyo ya
Muungano yahusuyo Zanzibar.
Hata hivyo mambo ya Muungano yaliongezwa kutoka 11 hadi 22
kutokana na mahitaji ya ndani ya nchi pamoja na mabadiliko yaliyokuwa
yanaendelea kutokea ulimwengini baada ya Muungano.
Mwaka 1985, jambo la 12 linalohusu sarafu na fedha kwa ajili ya
malipo na kurahisisha usimamizi wa fedha za kigeni na benki katika
Jamhuri ya Muunagno wa Tanzania, liliingizwa.
Kufuatia kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1967, mambo
matatu ya Muungano yaliyongezwa, ambayo ni leseni za viwanda na takwimu;
elimu ya juu; na usafirishaji wa anga.
Mwaka 1968, mambo ya maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta
yasiyochujwa ya magari na ama ya petroli na aina nyingine za mafuta au
bidhaa na gesi asilia yaliyongezwa kwenye orodha hiyo.
Aidha mambo ya Muungano yaliendelea kuongezeka hadi kufikia 21 kufuatia kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mwaka 1992 kufuatia mabadiliko ya mfumo wa siasa nchini suala la 22
la uandikishaji wa vyama vya siasa na mambo mengine yanayohusiana navyo
liliongezwa kwenye orodha hiyo.
MJADALA KUHUSU MUUNGANO
Katika
miaka hivi karibuni kumekuwa na mijadala mbalimbali kuhusiana na muundo
wa Muungano, baadhi wakitaka uwe wa zaidi ya serikali mbili, wengine
serikali moja, wapo wanaotaka Tanganyika iwe kivyake na Zanzibar
kivyake.
Hata hivyo hekima inaonyesha kwamba Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar unabaki kuwa ni fahari ya Watanzania, kwani mwelekeo wa dunia
katika nyanja mbalimbali, mataifa kuungana kwa ushirikiano wa aina
mbalimbali ni muhimu kuliko taifa moja kupambana kivyake.
Urejeaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika mwaka
1977, uwepo wa SADC, ECOWAS, COMESA, na jumuiya nyingine nyingi duniani
kote, ni vielelezo kwamba ushirikiano baina ya mataifa ni suala
lisilohitaji mjadala.
Ieleweke kwamba hakuna ushirikiano usio kuwa na matatizo kama
ilivyo kwa Muungano wa Tanzania, vivyo hivyo muungano mwingine kama vile
ya United Kingdom (UK), Uingereza na United States of America (USA) kwa
maana ya Marekani na United Arabs Emirate (UAE), nayo ina matatizo,
lakini hata mara moja mjadala juu ya matatizo hayo siyo kuvunja
ushirikiano bali kutatua na wale wanaotaka kuvunja hushughulikiwa
ipasavyo.
"Matatizo ya Muungano kama wa UK ni mabaya zaidi, na hata UAE
hawana ahueni, ila wanajua kwamba Muungano wao ni lazima. Wamarekani
wanapambana na watu wenye mawazo haya ya kuvunja miungano kwenye majimbo
ya Alaska, Hawaii na Texas na mwishowe wameamua kuweka kambi kubwa ya
jeshi la nchi kavu Texas; utitiri wa kambi za anga Alaska; na vituo
vikubwa kupindukia vya majini kule Hawaii. Hivi, hawa mabingwa wa
demokrasia wanapoamua kulinda nchi yao namna hii, unafikiri ni wajinga?
Walimwaga damu na waliyanunua majimbo haya na wamepitia shida kubwa,
ndiyo maana leo wanajidai," anaandika mchangiaji katika mjadala kuhusu
Muungano.
Ni vyema Watanzania wakati huu wa kusheherekea miaka 48 ya
Muungano, kila mmoja akajisikia ufahari wa kuwa na kitu kizuri
kilichoasisiwa na Waafrika wenyewe na kudumu kwa umri huo.
Mawazo ya kubaguana kwa sababu zisizo na msingi, pengine kukidhi matakwa
na wakati kama vile ya kibinafsi na kisiasa, yasipewe nafasi
kuisambaratisha nchi. Chambilecho wahenga, umoja ni nguvu utengano ni
udhaifu.
1 Comments:
Post a Comment
MDAU HUU NI UWANJA WAKO, ANDIKA MAONI YAKO HAPA UBADILISHANE MAWAZO NA WENZAKO. KUMBUKA MAONI YASILENGE KUCHAFUA HALI YA HEWA KIMAADILIMtumie mwenzako