NHC YAMWAGA MASHINE 640 ZA KUFYATULIA MATOFALI KWA WILAYA 160
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Rachel Kassanda
akikabidhi mashine nne kati ya 640 zenye thamani ya sh. mil. 288.za
kufyatulia matofali kwa Hassan
Soud Katibu wa kikundi cha Changamoto kwa niaba ya vikundi vingine vya
wilaya ya Ilala ambazo zimetolewa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),
wakati wa mkesha Ilala Bungoni, Dar es Salaam jana. Mashine hizo
zilikabidhiwa kwa Kassanda na Meneja wa NHC Kanda ya Ilala, Jackson Maagi (kushoto). Mashine 640 zitagawiwa katika halmashauri za wilaya 160 nchini.
Askari wa Kikosi cha FFU wakiulinda mwenge mara baada ya kuwasili Ilala Boma mahali ambapo ndiyo kituo ulipolala mwenge huo.
Meneja wa Shirika la Nyumba la
Taifa NHC Kanda ya Ilala, Jackson Maagi wa pili kutoka kushoto akiwa pamoja na
wafanyakazi wnzake kabla ya kukabidhi mashinne hizo jana.
Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC Bw. Jackson Maagi akizungumza wakati wa kukabidhi mashine hizo jana
………………………………………………………………………………..
HOTUBA FUPI YA MENEJA WA NHC ILALA KWA KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA
Ndugu kiongozi wa Mbio za mwenge,
Ninayo furaha kubwa sana kusimama mbele yenu na kuongea nanyi kama mwakilishi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge;
Shirika la Nyumba la Taifa lina mpango mkakati wake wa miaka mitano
ambao moja ya malengo yake sita makuu ni kuboresha taswira ya Shirika.
Katika utekelezaji wa lengo hili, Shirika lina sera ya huduma
kwa jamii ambayo imejikita katika kusaidia vijana kujiajiri. Ili
kuwezesha vijana kujiajiri, Shirika limeamua kuzisaidia Halmashauri za
Miji na Wilaya kote nchini mashine za kuwezesha vikundi vya vijana
kutengeneza matofali ya kujengea nyumba. Nchi yetu ina Halmashauri 160
na kila Halmashauri itapewa mashine 4 kwa ajili ya kusaidia vikundi vya
vijana. Katika mpango huu jumla ya mashine 640 zitatolewa na Shirika na
kugharimu shilingi 288,000,000/.
Aidha, kila Halmashauri itapatiwa shilingi laki tano (500,000/=)
kama mtaji kwa vijana kuanzia shughuli yao ya kutengeneza matofali.
Kadhalika, Shirika limegharamia shilingi 800,000/= kwa kila Halmashauri
kwa ajili ya kuwalipa wakufunzi kutoka VETA wanaotoa maelekezo kwa
vijana namna ya kutumia mashine hizo.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge,katika kutekeleza mradi huu
jumla ya shilingi milioni mia saba (700,000,000/=) zitatumika. Aidha,
tunatarajia kuwa ajira zaidi ya 8,000 za moja kwa moja na ajira nyingine
zaidi ya 200,000 zisizo za moja kwa moja zitapatikana.
Katika mpango huu kila Wilaya inatakiwa kuwa na vijana 40
watakaokuwa katika vikundi vya watu 10 kila kimoja. Msaada huu ni mkubwa
lakini kutokana na ukubwa wa tatizo la ajira jitihada zaidi kutoka kwa
wadau mbalimbali zinatakiwa. Ni matarajio yetu kuwa taasisi nyingine ama
mtu mmoja mmoja atashiriki kukwamua vijana hawa.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge, kupitia maadhimisho haya,
Shirika linatoa mashine nne (4) kwa vikundi 4 vya vijana vilivyoundwa
katika wilaya ya Ilala ambapo kila kikundi kina jumla ya vijana10
watakaotumia mashine moja. Hivyo jumla ya vijana 40 katika Wilaya hii
watapata ajira kutokana na mashine hizi.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge, mwisho Shirika linatoa rai kwa
Taasisi za serikali, mashirika ya umma, binafsi na watu mbalimbali,
kuunga mkono juhudi za Serikali za kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
Ni matumaini yetu kuwa tutawaunga mkono kwa kununua matofali yao ama
kusaidia upatikanaji wa mashine nyingine zaidi ili wengine ambao
hawajafikiwa na mradi huu wafikiwe na wapate kufaidika.
Kipekee tunaomba Serikali za Mitaa (kwa maana ya Halmashauri
zetu za wilaya, miji, manispaa ama jiji) wawe ni wanunuzi wakuu wa
matofali yatakayotengenezwa na vikundi hivi vya vijana ambayo ni ya
gharama nafuu ili kusaidia miradi mbalimbali ya ujenzi na kuwaongezea
kipato chao. Tunawaomba pia msaidie kusimamia mradi huu ili uweze kuwa
endelevu.