Ndege aliyoizindua Nyalandu mbovu
*Ni zawadi ya Ujerumani kwa ajili ya kupambana na ujangili
*Yadaiwa ipo JNIA kwa miaka mitatu, imepakwa rangi juzi tu
*Haijawahi kuruka tangu itue Dar es Salaam kutoka ughaibuni
NA MWANDISHI WETU, Dar
WAKATI
dunia ikiwa katika vita ya kupambana na ujangili, juzi usiku, Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alizindua ndege iliyotolewa na
Ujerumani kwa ajili ya mapambano hayo.
Ndege
hiyo ilizinduliwa mwishoni mwa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa
Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Hata
hivyo, taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka kwa vyanzo vyake vya
uhakika zimeweka wazi kuwa ndege hiyo inayotarajiwa kutumiwa na Wizara
ya Maliasili na Utalii kupambana na ujangili, ni mbovu.
Sherehe za uzinduzi huo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, watendaji wa wizara husika na waandishi wa habari.
“Ndege
hii (iliyozinduliwa), ipo hapa hapa uwanjani (JNIA) kwa kama miaka
mitatu hivi; haijawahi kuruka tangu ifike hapa, sasa iweje leo
ikabidhiwe kwa serikali kupambana na ujangili? Hapa kuna kitu hakijakaa
vyema,” alisema mtoa habari wetu, Ofisa wa Uwanja wa Ndege ambaye ni
wazi hatutoweza kuandika jina lake gazetini kwa sasa.
Alisema
kilichofanyika kabla ya kuzinduliwa kwa ndege hiyo hapo juzi, ni kupaka
rangi iweze kuonekana kama mpya, au walau inaweza kufanya kazi, wakati
ukweli wa ndege hiyo unajulikana.
“Kazi
inayotarajiwa kwenda kufanywa na ndege hiyo ni kubwa kuliko uwezo wake.
Ikitumika, kuna uwezekano mkubwa wa maafa kutokea na Watanzania wenzetu
kupoteza maisha.
“Huu
sasa ni kuuanika umasikini wa nchi yetu hata pasipo na sababu. Ndege
hii haijawahi kufanya safari yoyote kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Kwanini maliasili wakubali kupokea ‘kimeo’,” alisema na kuhoji ofisa
mwingine uwanjani hapo.
Akizungumza
na Raia Tanzania jana, mwanachi mmoja aliishangaa Serikali kushindwa
kununua ndege rasmi kwa ajili ya kupambana na majangili, kama kweli
inahitajika, badala ya kupokea ndege iliyotelekezwa uwanjani kwa miaka
miwili au mitatu.
“Umasikini
ni kitu kibaya sana, unaweza kupewa msaada bandia huku unashangilia.
Kwa nini wizara isitumie wataalamu wa masuala ya ndege waliopo nchini
kuikagua kabla ya kuzinduliwa?,” alihoji.
Hata
hivyo, pamoja na unyeti wa suala hili, bado Waziri wa Maliasili na
Utalii, Nyalandu na katibu mkuu wake, Maimuna Tarishi, hawakutoa
ushirikiano kwa mwandishi wa habari hii.
Nyalandu,
alipopigiwa simu ya mkononi kwa mara ya kwanza saa 6.49 mchana,
hakupokea simu; na alipoandikiwa ujumbe mfupi wa maandishi dakika chache
baadaye, alijibu kwa kifupi ‘I am in a meeting’.
Na alipotafutwa tena saa 8.29 mchana, bado hakupokea na kutuma ujumbe wenye maneno yale yale, kwamba yuko kwenye mkutano.
Wadadisi
wa mambo jijini Dar es Salaam, wamekuwa wakihoji uhalali wa kutumia
nguvu nyingi kupambana na majangili ambao serikali imeshaitangazia dunia
kuwa inawafahamu, na kwamba kinara wao anaishi Arusha.
Mmoja
kati yao, aliliambia Raia Tanzania kuwa ni ajabu kwa serikali kupokea
zawadi za magari na ndege kwa ajili ya kupambana na majangili
wanaofahamika.
No comments:
Post a Comment